77 MÜRSELAT

 • 77:1

  Naapa kwa zinazo tumwa kwa upole!

 • 77:2

  Na zinazo vuma kwa kasi!

 • 77:3

  Na zikaeneza maeneo yote!

 • 77:4

  Na zinazo farikisha zikatawanya!

 • 77:5

  Na zinazo peleka mawaidha!

 • 77:6

  Kwa kuudhuru au kuonya,

 • 77:7

  Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka yatakuwa!

 • 77:8

  Wakati nyota zitakapo futwa,

 • 77:9

  Na mbingu zitakapo pasuliwa,

 • 77:10

  Na milima itakapo peperushwa,

 • 77:11

  Na Mitume watakapo wekewa wakati wao,

 • 77:12

  Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda huo?

 • 77:13

  Kwa siku ya kupambanua!

 • 77:14

  Na nini kitakacho kujuulisha siku ya kupambanua ni nini?

 • 77:15

  Ole wao, siku hiyo hao wanao kanusha!

 • 77:16

  Kwani hatukuwaangamiza walio tangulia?

 • 77:17

  Kisha tukawafuatilizia walio fuatia?

 • 77:18

  Ndio kama hivi tuwatendavyo wakosefu!

 • 77:19

  Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!

 • 77:20

  Kwani hatukukuumbeni kwa maji ya kudharauliwa?

 • 77:21

  Kisha tukayaweka mahali pa utulivu madhubuti?

 • 77:22

  Mpaka muda maalumu?

 • 77:23

  Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria.

 • 77:24

  Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!

 • 77:25

  Kwani hatukuifanya ardhi yenye kukusanya

 • 77:26

  Walio hai na maiti?

 • 77:27

  Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenye kuthibiti, na tunakunywesheni maji matamu?

 • 77:28

  Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!

 • 77:29

  Nendeni kwenye adhabu mliyo kuwa mkiikanusha!

 • 77:30

  Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu!

 • 77:31

  Hakikingi moto, wala hakiwaepushi na mwako.

 • 77:32

  Hakika Moto huo unatoa macheche kama majumba!

 • 77:33

  Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano!

 • 77:34

  Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!

 • 77:35

  Hii ni siku ambayo hawatatamka kitu,

 • 77:36

  Wala hawataruhusiwa kutoa udhuru.

 • 77:37

  Ole wao siku hiyo hao walio kanusha!

 • 77:38

  Hii ndiyo siku ya kupambanua. Tumekukusanyeni nyinyi na walio tangulia.

 • 77:39

  Ikiwa mnayo hila, nifanyieni hila Mimi!

 • 77:40

  Ole wao siku hiyo hao walio kanusha!

 • 77:41

  Hakika wachamngu watakuwa katika vivuli na chemchem,

 • 77:42

  Na matunda wanayo yapenda,

 • 77:43

  Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda.

 • 77:44

  Hakika ndio kama hivyo tunavyo walipa watendao mema.

 • 77:45

  Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!

 • 77:46

  Kuleni na mjifurahishe kidogo tu. Hakika nyinyi ni wakosefu!

 • 77:47

  Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!

 • 77:48

  Na wakiambiwa: Inameni! Hawainami.

 • 77:49

  Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!

 • 77:50

  Basi maneno gani baada ya haya watayaamini?

Paylaş
Tweet'le